Zinazobamba

ZITTO KABWE AAPA KUPAMBANA NA RAIS MAGUFULI,AMWITA RAIS WA MUHULA MMOJA,SOMA HAPO KUJUA



Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania


ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo leo ametoka hadharani na kusema, ‘Rais John Magufuli ajiandae kuongoza nchi kwa muhula moja,’ anaandika Hamisi Mguta.
 
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini amemtabiria Rais Magufuli kuwa, ataweka historia ya kuwa rais wa muhuma mmoja kwasababu Watanzania hawatamvumilia kuwatawala kwa kuwaburuza kidikteta.

Zitto ameibuka leo ikiwa ni siku moja baada ya vyombo vya habari kuripoti kwamba, kiongozi huyo wa upinzani hajulikani alipo.
Hata hivyo amesema kuwa, alipata taarifa za kutaka kukamatwa kwake na kwamba, alichokifanya ni kuonesha kuwa hawezi kukamatwa ‘ovyo ovyo.’

Zitto ametoa kauli hiyo leo mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo amedai kuwa Rais Magufuli ameanza na vyama vya siasa kuonesha udikteta wake, kitu ambacho hakifai katika demokrasia ya Tanzania.

“Nawahakikishia, akimalizana na vyama vya siasa atahamia kwenu wanahabari, tumkatalie,” amewaambia waandishi wa habari waliokuwapo katika mkutano huo.

Hata hivyo amesema kuwa, hajui kwanini polisi walizuia kongamano la chama chake jana lililopanga kuchambua Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/17 katika Jengo la Millenium Towers, Kijitonyama Dar es Salaam.

”Kama serikali haifanyi sawasawa ni wajibu wetu kuwakosoa, na tutawakosoa kama tulivyokuwa tukifanya kwenye serikali iliyopita…serikali ya sasa haina uvumilivu,” amesema Zitto.

Zitto amesema, ili kupambana na ufisadi nchini ni lazima Rais Magufuli ampe nguvu ya kiutendaji Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Seriali nchini (CAG).
Amesema “CCM wanapaswa kumdhibiti Rais Magufuli na wasipomdhibiti, sisi na Watanzania tutamdhibiti.”
Amesema, Jumamosi watu wao wa usalama walimjulisha kuwa Jeshi la Polisi linamsaka ambapo pia walikwenda nyumbani kwake wakiwa na magari manne ili kumtia nguvuni.
“Jumanne iliyopita Kamishna Wambura alinipigia simu kuniomba nifike polisi lakini hii ya Jumaamosi walikuwa wanataka kunivizia, hatufahamu watawala wanaogopa nini mpaka kuzuia mikutano ya wanasiasa,” amesema Zitto.
Zitto amesema, suala la kumkamata Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mwanza jana kwa sababu ya kawasalimia wananchi, ni uvunjwaji na ukiukwaji mkubwa wa utawala wa kidemokrasia na kwamba, hizo ni tabia za kidikteta.
”Tunalaani tabia za kidikteta za Rais Magufuli, ndio maana Magufuli ziara yake ya kwanza alifanya Rwanda, tumegundua kuwa alikwenda kujifunza namna ya kudhibiti Demokrasia na kuongoza kidikteta,” amesema Zitto.
Amesema, hawatakaa kimya hata kama Rais Magufuli ataamua kuwafunga na kuwa, ‘akimfunga Zitto, watazaliwa wakina Zitto wengine,’
Amedai kuwa IGP Ernest Mangu ameagizwa na Rais Magufuli amkamate huku akisema “siwezi kukamatwa bila kufuata utaratibu.”
”Karibuni kesho saa tisa kwenye kongamano letu, hatuwezi kuacha kufanya siasa, lazima tuendelee kufanya siasa, mmeudhuria mikutano yetu hamjaona hata sisimizi amekanyagwa.
”Sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 inaruhusu vyama vya siasa kufanya siasa, makongamano na mikutano ni sehemu ya siasa, hatuhitaji kuomba kibali na tutaweka utaratibu ili Watanzania wengi zaidi waweze kushiriki kwenye kongamano,” amesema Zitto.
Amesema, polisi hawana mamlaka ya kisheria kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na kwamba, anaipongeza Chadema kufungua kesi ya kikatiba Mwanza huku nao wakidhamiria kufungua kesi ya namna hiyo jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni